Naibu Rais Rigathi Gachagua anasema Kenya itakuwa mwenyeji wa kongamano litakalowajumuisha wafanyabiashara kutoka Misri kuhusu uwekezaji.
Gachagua anasema wakati umewadia kwa nchi hizo mbili kufanya uwekezaji zaidi wa pamoja kwa manufaa ya kiuchumi ya pande mbili.
Alizungumza hayo alipokutana na Balozi wa Misri nchini Kenya Wael Attiya katika afisi yake iliyopo Harambee House Annex jana Alhamisi.
Kauli za Naibu Rais zilifuatia ombi la balozi huyo aliyetaka kuwepo mkutano kati ya Kenya na wafanyabiashara kutoka Misri kuhusu uwekezaji.
Kulingana na Balozi Attiya, wafanyabiashara kutoka Misri wako tayari kuwekeza humu nchini.
Kulikuwa na mipango ya Kenya na Misri kuandaa kongamano la uwekezaji mjini Cairo mwakani, lakini Balozi Attiya aliomba kongamano hilo liandaliwe mapema jijini Nairobi.
“Tunaweza tukaharakisha kuandaliwa kwa kongamano la biashara na timu yetu katika Wizara ya Mambo ya Nje haraka iwezakanavyo,” alisema Naibu Rais.
Aliongeza kuwa Kenya iko tayari kwa uwekezaji wa pamoja katika njanja za kilimo, elimu, teknolojia na utalii miongoni mwa zingine.
“Kampuni zetu zina shauku ya kufanya kazi na Kenya katika uwekezaji wa pamoja. Kuna shauku kubwa. Mwaka jana, zaidi ya kampuni 20 kutoka nchini Misri ziliitembelea Kenya kuangazia nafasi zilizopo,” alisema Balozi Attiya.