Kenya, Colombia kuimarisha uhusiano

Martin Mwanje
1 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Jumatatu jioni amekutana na Makamu Rais wa Colombia Francia Elena Marquez Mina anayezuru nchini katika ofisi yake iliyopo Harambee House Annex.

Mkutano huo unakuja kabla ya Gachagua kufanya ziara rasmi nchini Colombia wiki ijayo.

Wakati wa mkutano kati yao, viongozi hao wawili walisifia uhusiano unaoimarika kati ya nchi hizo na kuahidi kuuimarisha hata zaidi na kuhakikisha nchi zote mbili zinatafuta nyanja za ushirikiano wa biashara hasa katika kilimo hususan sekta ya kahawa.

Mina anayehudhuria Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi anazuru Kenya kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi mitatu.

Gachagua anasimamia mabadiliko katika sekta ya kahawa na amepangiwa kusafiri pamoja na wakulima wa kahawa kuelekea nchini Colombia ili kujionea matumizi ya teknolojia iliyoboreshwa katika kilimo na pia kujifunza njia bora za uongezaji thamani.

Mina aliupongeza uongozi wa Kenya kwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi akisema linatoa jukwaa la kuangazia changamoto zinazoikumba Afrika kuhusiana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuzitafuta suluhu changamoto hizo.

Alielezea imani kuwa kongamano hilo litasaidia kutafuta suluhu madhubuti.

Viongozi hao waliahidi kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Share This Article