Halmashauri ya usambazaji dawa na vifaa vya matibabu hapa nchini( KEMSA), imeagizwa kununua bidhaa za matibabu zinazotengenezewa hapa nchini.
Akitoa agizo hilo, Rais William Ruto alisema KEMSA imetengewa Shilingi bilioni mbili za ziada, ili kuimarisha uwezo wake wa kununua bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.
Rais alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani ili kuongeza upatikanaji na uwezo wa kumudu bidhaa za afya na teknolojia.
Hii, alielezea, itaharakisha utimilifu wa Huduma ya Afya kwa Wote, kubuni ajira, kuongeza mapato kupitia kodi na kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Utawala wangu umejitolea kuhakikisha kuwa, kufikia 2026, angalau asilimia 50 ya dawa zilizoorodheshwa katika Orodha ya Dawa Muhimu za Kenya zitatengenezwa na kupatikana nchini,” alisema.
Rais alisema hayo wakati wa Maonyesho ya Utengenezaji wa Bidhaa za Afya humu nchini katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa KICC jijini Nairobi.
Hapo awali, alitembelea Kiwanda cha dawa cha Square Pharmaceuticals katika Eneo la Uchakataji Kiuchumi la Athi River katika Kaunti ya Machakos.
Rais alisema Serikali imejipanga kutokomeza rushwa katika Wizara ya Afya na mchakato wa manunuzi katika KEMSA.
“Ununuzi katika KEMSA hautaendeshwa tena na wachuuzi ambao wanaendelea kubadilisha viwango vya bidhaa za dawa ili kutawala soko,” alisema.
Kiongozi wa Nchi alisema Serikali inashughulikia sheria ambayo itaweka mfumo wa udhibiti na sera unaohitajika ili kutoa motisha kwa wawekezaji katika maduka ya dawa na kusaidia utoaji wa Huduma ya Afya kwa Wote.
“Lazima niwapongeze bunge, jana vipande viwili vya sheria vilihitimishwa, na hadi wiki ijayo watahitimisha vingine viwili,” alisema.
Rais Ruto alisema kuna mipango ya kuifanya Kenya Power kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za umeme kwa watengenezaji wa humu nchini ili kupunguza gharama ya uzalishaji.
Alisema Serikali imeondoa kodi kwenye utengenezaji wa chanjo za wanyama na binadamu ili kuinua zaidi tasnia ya dawa.
Rais Ruto aliendelea kusema kuwa Serikali itaongeza ufadhili wa majaribio ya kimatibabu katika Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya (KEMRI) ili kuimarisha utafiti, maendeleo na uvumbuzi.
Viongozi waliokuwepo ni Mawaziri Susan Nakhumicha, Rebecca Miano, na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.