Taasisi ya utafiti wa kimatibabu nchini (KEMRI) imetangaza kwamba imeandaa maabara maalum kote nchini kufuatia chamko la ugonjwa wa virusi vya Marburg (MVD) nchini Rwanda.
Mkurugenzi mkuu wa KEMRI, Profesa Elijah Songok alisema kuwa maabara hayo yatatumiwa kufanyia uchunguzi sampuli kwa haraka na kwa ufanifu ili kuimarisha juhudi za nchi hii za kukabiliana na ugonjwa huo.
Mnamo tarehe 27 mwezi uliopita wizara ya afya nchini Rwanda iliripoti visa vya maambukizi ya ugonjwa huo kwenye vituo vya afya nchini humo.
Kufikia tarehe 2 mwezi Oktoba, Rwanda ilikuwa imekanili visa 36 vilivyothibitishwa kwenye maabara vikiwemo vifo kutokana na ugonjwa huo.
Yamkini wagonjwa 19 kati ya hao ni wahudumu wa afya ambapo wengi wao hufanya kazi kwenye vitengo vya wagonjwa mahututi.
Ugonjwa wa MVD huenda kwa haraka sawia na ule wa Ebola, na kwa sasa hakuna matibabu au chanjo yoyote iliyoidhinishwa dhidi ya ugonjwa huo.
Dalili za virusi hivyo ni pamoja na homa, kibaridi, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, vipele, maumivu ya kifua, maumivu ya koo, kuhara, kutapika, maumivu ya tumbo na kuvuja damu.