Taasisi ya Utafiti wa Misitu nchini, KEFRI imezindua mradi wa shilingi milioni 30 unaolenga kufikia usimamizi endelevu wa spishi ya Prosopis juliflora.
Lengo la mradi huo ni kubuni nafasi kijani za ajira na kuboresha maisha ya wakazi wa Turkana Magharibi.
Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Kazi Duniani, ILO, unalenga maeneo ya Kakuma, Kalobeyei, Songot, Nanam, Letea, Pelekech na Lopur na utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Ukitumia teknolojia bora za tabia nchi, mradi huo unakusudia kuibadilisha spishi hiyo inayosambaa kuwa yenye manufaa kiuchumi. Shughuli muhimu zinajumuisha utengenezaji wa kaboni kwa ajili ya uzalishaji wa matofali yaliyotengenezwa kwa mavumbi ya mkaa na mkaa pamoja na mitungo ya thamani ya mkaa.
“Kupitia utafiti, mradi huo utaunda jukwaa kwa ajili ya mipango inayoongozwa na jamii, na kuwezesha uzalishaji wa malisho ya mifugo ya thamani ya juu kutoka kwa maganda na vijiti vya Prosopis kwa ajili ya kuuzwa, na kwa hivyo kuwawezesha kiuchumi watu waliolengwa,” amesema Patrick Mwirigi, Mkurugenzi Msaidizi wa KEFRI katika eneo la Turkana.
Kama sehemu ya uzinduzi huo, wanachama 30 kutoka kikundi cha Nyuki cha Kakuma, zikiwemo jamii mwenyeji na za wakimbizi, zilipokea mafunzo juu ya mitungo mbalimbali ya thamani ya Prosopis.
Mafunzo hayo yalijumuisha uzalishaji wa sabuni, mishumaa, vipodozi na kutafiti manufaa ya kitabibu ya bidhaa za Prosopis kama vile asali na nta.