KCSE 2024: Matokeo ya watahiniwa 840 yafutwa

Martin Mwanje
1 Min Read
Julius Ogamba - Waziri wa Elimu

Watahiniwa 840 wana kila sababu ya kuhuzunika baada ya matokeo yao mtihani wa kidato cha nne, KCSE 2024 kufutwa. 

Akizungumza wakati wa kutangazwa kwa matokeo hayo, Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika watahiniwa hao walijihusisha katika visa vya udanganyifu.

Uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na visa 2,829 vya udanganyifu kwenye mtihani huo.

Hii ina maana ya kwamba watahiniwa husika watasubiri hadi uchunguzi ukamilike kabla ya kufahamu hatima yao.

Uchunguzi kubaini ikiwa watahiniwa hao walihusika katika visa vya udanganyifu utafanywa kwa kipindi cha siku 30 kuanzia leo Alhamisi matokeo yalipotangazwa.

Wanataaluma wote waliokodiwa kuwezesha kufanyika kwa udanganyifu huo nao watachukuliwa hatua.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa leo Alhamisi,watahiniwa 1,693 walipata Gredi ya A.

Watahiniwa 246,391 walifuzu kujiunga na vyuo vikuu baada ya kupata Gredi ya C+ na zaidi.

Jumla ya watahiniwa 962,512 walifanya mtihani wa KCSE mwaka 2024.

Kati ya watahiniwa hao, 480,310 walikuwa wa kiume na 482,202 wa kike.

Hii ni mara ya kwanza kwa idadi ya watahiniwa wa kike kuzidi ile ya watahiniwa wa kiume nchini.

Watahiniwa wanaweza wakapata matokeo yao kwa kubonyeza linki ifuatayo: https://results.knec.ac.ke.

Watahiniwa watahitajika kuweka nambari na jina lao la usajili wa mtihani huo ili kupokea matokeo.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *