KCSE 2023: Watahiniwa wote shule ya upili ya Oruba, Migori wazoa alama za D na E, walalamika

Martin Mwanje
1 Min Read

Watahiniwa wa shule ya upili ya wavulana ya Oruba katika kaunti ya Migori wamelalamikia matokeo duni waliopata katika mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2023, KCSE wakidai si ya kweli. 

Kati ya watahiniwa 75 waliofanya mtihani huo shuleni hapo, ni wawili pekee waliopata alama ya C-.

Wengine waliambulia alama za D na E.

Hali iliyowalazimu watahiniwa hao kuandamana hadi afisi ya Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti ya Migori kuelezea kutoridhika kwao na matokeo hayo.

Kulingana nao, hawajawahi kupata matokeo kama hayo wakati wa kipindi cha miaka minne ya masomo na matokeo hayo ni ya kusikitisha.

Jaribio lao la kutaka kuzungumza na mwalimu mkuu, naibu mwalimu mkuu na hata mwalimu anayesimamia mitihani shuleni hapo ziliambulia nunge kwani hawakupatikana hata kwenye simu.

Aidha, hakuna aliyekuwa katika afisi ya elimu isipokuwa tu afisa wa ngazi ya chini aliyekataa kuwahutubia wanahabari.

Afisa huyo badala yake aliwataka wanafunzi hao kuwasilisha lalama zao kwa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini, KNEC.

Results

 

Share This Article