Shirika la utangazaji nchini Kenya,KBC limenunua haki miliki za kupeperusha kwenye runinga na kutangaza michuano yote 52 ya fainali za kuwania kombe la AFCON makala ya 34 nchini Ivory Coast.
KBC itapeperusha mechi hizo kupitia runinga ya Y254 na KBC Channel 1, huku pia likitangaza mechi zote kupita idhaa zote 13 za redio kati ya Januari 13 na Februari 11 mwaka huu.
Hafla ya kutangaza uzinduzi wa haki miliki za AFCON, imeandaliwa Ijumaa na kuongozwa na waziri wa Michezo Ababu Namwamba.
Mataifa 24 yanashiriki patashika hiyo huku Senegal wakitetea taji waliyotwaa mwaka 2021 kwa mara ya kwanza.
Mechi hizo zitaandaliwa katika viwanja sita vilivyo katika miji 5 tofauti huku, jiji kuu la Abidjan likiwa na nyuga mbili.
KBC pia itapeperusha mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika,Kombe la Shirikisho ,Ligi ya Mabingwa ya wanawake na mechi za kufuzu kwa kombe la AFCON mwaka 2025.