KBC kuendelea kurusha mubashara vikao vya bunge

Martin Mwanje
2 Min Read
Clement Nyandiere - Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Pamoja za Bunge (PJS)

Bunge litaendelea kulitumisha Shirika la Utangazaji nchini, KBC kurusha mubashara vikao vya bunge. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Pamoja za Bunge (PJS) Clement Nyandiere.

Nyandiere amesisitiza kuwa bunge litaendelea kutumia KBC kurusha mubashara matangazo yake ya vikao vya bunge na vile vya kamati za bunge.

Alisisitiza wajibu muhimu wa bunge kuunga mkono azima ya KBC kurusha matangazo kila pembe ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu huyo aliyasema hayo alipofika mbele ya Kamati ya Uhasibu ya Bunge la Taifa kuangazia ripoti ya Mkaguzi Mkuu ya mwaka wa fedha uliomalizika wa Juni 30, 2022.

Alikiri kuwa bunge linadaiwa deni kubwa na KBC.

Licha ya deni hilo, Nyandiere alisema KBC imekuwa ikirusha mubashara matangazo ya bunge kwa kiwango kidogo cha fedha, na kuongeza kuwa msaada wa bunge kwa shirika hilo ni muhimu ili kufanikisha shughuli za shirika hilo kurusha matangazo yake kote nchini.

“KBC inasaidiwa kwa kiasi kikubwa na bunge katika utenda kazi wake. Lakini kama shirika la utangazaji la umma, tunaamini bunge lina wajibu wa kuisaidia KBC kuendelea kurusha matangazo yake kote nchini. KBC, ndio shirika la pekee, kupitia idhaa zake za redio na runinga,  ambalo linarusha matangazo yake kote nchini, kila sehemu ya nchi,” aliongeza Nyandiere.

Hata hivyo, alisema ingawa bunge linadhamiria kurusha matangazo yake lenyewe siku zijazo, miundombinu yake ya sasa ya urushaji matangazo hayo haitoshelezi huku fedha zinazokadiriwa kuwa bilioni 2 zikihitajika ili kupata miundombinu ya kisasa.

“Hatujafanikiwa kupata ufadhili wa kutosha kuendeleza miundombinu ambayo italiwezesha bunge kutangaza matangazo yake kikamilifu. Mpango wa muda mrefu umetayarishwa, lakini kwa sasa, tunaitegemea KBC kufikia umma kwa njia bora na kwa gharama nafuu,” alisema Nyandiere.

“Kwa sasa, kushirikiana na KBC kunasalia njia bora zaidi na yenye gharama nafuu ya kuendelea kuwasiliana na umma.”

 

Share This Article