Timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars itashuka ugani Franceville nchini Gabon leo Alhamisi usiku kwa mchuano wa kwanza wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 dhidi ya Gabon.
Mchuano huo utang’oa nanga saa moja usiku majira ya Afrika Mashariki.
Mechi hiyo ya kundi F itakuwa muhimu kwa timu zote katika azima ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2026 katika mataifa ya Marekani, Mexico na Canada.
Kenya inayofunzwa na kocha Engin Firat iliondoka nchini jana Jumatano kwa pambano hilo.
Harambee Stars watakwangurana na Gabon kwa mara ya tano baada ya Kenya kuwashinda Gabon bao moja kwa nunge mwezi Januari mwaka 1998, kabla ya Gabon kuishinda Kenya bao moja kwa nunge katika mechi ya marudio kufuzu kombe la Afrika.
Timu hizo pia ziliwekwa katika kundi moja kufuzu kwa fainali za kombe la Afrika mwaka 2002, Kenya wakitoka sare ya bao 1 kwa moja mjini Libreville, kabla ya Harambee Stars kuipiga Gabon 2-1 katika mechi ya marudio ugani Nyayo.
Kenya inaorodheshwa ya 110 huku Gabon ikiwa ya 86 katika msimamo wa FIFA.
Kundi F pia linajumuisha Ivory Coast, Ushelisheli, Burundi na Gambia huku viongozi wa kundi wakijikatia tiketi kwa dimba la Komba la Dunia.