Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani na naibu wake Chirema Kombo wamezindua ukarabati wa mradi wa maji wa Sagalato na bwawa la Bofu, katika eneo la Kibandaongo na Kasemeni mtawalia, kaunti ndogo ya Kinango.
Miradi hiyo ambayo ni kwa ushirikiano kati ya kaunti ya Kwale na serikali ya taifa, inalenga kutatua changamoto la ukosefu wa maji katika kaunti ndogo za Kinango, Samburu na Lungalunga na pia kufanikisha kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Kulingana na Gavana huyo, ukarabati wa mradi wa maji wa Sagalato, utahusisha kuondoa vichaka vilivyo karibu, ujenzi wa vibanda vya kuuza maji na sehemu za mifugo kunywa maji.
Hadi kufikia sasa, serikali ya kaunti ya Kwale, imejenga zaidi ya mabwawa 17, vidimbwi 40 na kilomita 573 ya mifereji ya kusambaza maji.
“Tunapoendelea na ujenzi wa mabwawa, nahimiza kila mmoja wetu tuendelee kupanda miti zaidi ili tuepushe uharibifu zaidi unaosababishwa na mabadiliko ya Tabia Nchi,” alisema Achani.
Kwa upande wake, naibu Gavana wa kaunti hiyo Josphat Chirema Kombo, alisema kaunti hiyo itaendelea kutafuta suluhu kuhusu ukosefu wa maji ya kutosha katika kaunti hiyo, ili kuhakikisha wakazi wanapata maji ya matumizi nyumbani na kunyunyiza mashamba.