Serikali ya kaunti ya Kisumu imesitisha ujenzi wa soko la Uhuru Business Complex ambao umekuwa ukiendelea tangu mwaka 2019.
Soko hilo lilikuwa linajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 600 na iliyokuwa serikali kuu ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ili kuwasaidia wafanyabiashara waliokuwa wamebomolewa vibanda vyao.
Hatua ya kusimamisha ujenzi huo iliafikiwa kwenye kikao cha kamati ndogo ya baraza la mawaziri la kaunti, tarehe 21 mwezi huu kuhusu ushirikiano wa ujenzi wa soko hilo kati ya serikali ya kaunti ya Kisumu na Shirika la Reli nchini.
Naibu Gavana wa kaunti ya Kisumu Dkt. Matthews Owili ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema uamuzi huo uliafikiwa na wanachama wote baada ya kukadiria sababu kadhaa.
Yamkini baadhi ya sababau za kusitishwa kwa ujenzi wa soko hilo ni hatua ya wakandarasi walaghai kutwaa shughuli ya ujenzi na visa kadhaa vya ufisadi.