Serikali ya kaunti ya Embu, kuanzia Januari mwaka ujao, itaanzisha mradi wa lishe shuleni kwa wanafunzi wa chekechea,ECDE.
Kulingana na Gavana wa kaunti hiyo Cecily Mbarire, katika awamu ya kwanza wanafunzi hao watapewa uji kama kiamsha kinywa, kabla ya mradi huo kupanuliwa zaidi.
Gavana huyo alisema mpango huo unalenga kuhakikisha wanafunzi wansalia shuleni, ili kuboresha masomo yao.
“Mpango huu utahakikisha wanafunzi kutoka familia masikini wanaenda shuleni,” alisema Gavana huyo.
“Tunazindua mpango huu wa kuwapa wanafunzi uji, ili kuimarisha lishe ya wanafunzi, huu ukiwa ni sehemu ya kujitolea kwetu kufanikisha upatikanaji wa elimu bora ya ECDE,” alisema Mbarire.
Alielezea mipango ya kujenga madarasa mapya ya ECDE katika kaunti hiyo, huku akitoa wito kwa wawakilishi wadi kupiga jeki juhudi hiyo kupitia hazina ya kustawisha wakilishi wadi.
“Ikiwa kila mwakilishi wadi atajenga darasa moja au mawili kila mwaka, tutakuwa na madaras mengi kufikia mwaka 2027,” alidokeza Mbarire.