Bingwa wa Olimpiki katika urushaji nyundo Ethan Katzberg kutoka Canada anatarajiwa kurejea mwezi ujao kutetea taji la Kip Keino Classic wakati wa makala ya saba uwanjani Nyayo.
Katzberg, ambaye pia ni bingwa wa dunia mara mbili, alitwaa ubingwa mwaka jana katika uwanja wa Ulinzi, kabla ya kutetea taji lake la Dunia jijini Tokyo, Japani mwezi Septemba.
Aidha, kulingana na waandalizi, maafisa kutoka Shirika la Riadha Duniani wanatarajiwa kuwasili nchini mapema wiki ijayo kukagua uwanja wa Nyayo kwa maandalizi ya mashindano hayo ya tarehe 24 mwezi ujao.
Mashindano hayo yatakuwa ya mzunguko wa pili ya kiwango cha nembo ya dhahabu na yatafuatia mkondo wa kwanza utakaofanyika nchini Australia baina ya tarehe 27 na 28 mwezi huu.