Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kiprono Ronoh ameongoza usambazaji wa awamu ya kwanza ya mifuko 47,300 ya mbolea aina ya NPK, kwa upanzi wa msimu wa mvua za vuli za mwezi Oktoba hadi Disemba.
Mbolea hiyo itasambaziwa wakulima wapatao 650,000 wa majani chai, na ni sehemu ya kwanza ya tani 97,000, za mbolea zilizokuwa zimeagizwa na shirika ya ustawishaJi majani chai nchini, KTDA.
Shehena ya pili ya mbolea inatarajiwa kutua hapa nchini katika kipindi cha majuma mawili yajayo.
Katibu Ronoh amekariri kujitolea kwa serikali kuimarisha na kuwapiga jeki wakulima kupitia kwa mbolea hiyo ya bei nafuu, ili kuongeza uzalishaji, katika juhudi za kufanikisha uwezo wa taifa hili kujitosheleza kwa chakula.
Mbolea hiyo itauzwa kwa bei ya shilingi 2,500, kwa wakulima waliosajiliwa.