Katibu Raymond Omollo azuru kaunti ndogo ya Makadara kukagua kazi inayoendelea ya Climate WorX

Ziara ya Omollo katika eneo hilo karibu na kituo cha polisi cha Lunga Lunga, kaunti ndogo ya Makadara kaunti ya Nairobi ni dhihirisho la kujitolea kwa wizara kukuza hulka endelevu za kimazingira na ustahimilivu wa jamii.

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu wa usalama wa ndani na utawala wa kitaifa Raymond Omollo, leo amezuru eneo ambako kazi za kutunza mazingira chini ya mpango wa Climate WorX mtaani zinaendelea.

Ziara ya Omollo katika eneo hilo karibu na kituo cha polisi cha Lunga Lunga, kaunti ndogo ya Makadara kaunti ya Nairobi ni dhihirisho la kujitolea kwa wizara kukuza hulka endelevu za kimazingira na ustahimilivu wa jamii.

Wakati wa ziara hiyo, Omollo aliangazia jukumu muhimu linalotekelezwa na mpango wa Climate WorX mtaani, mpango bunifu unaolenga kushughulikia changamoto za hali ya anga kupitia suluhisho za jamii.

Mpango huo umejikita katika kuimarisha ustahimilivu wa hali ya anga, kuhimiza uendelevu na kukuza ushirikiano kwa ajili ya urejesho wa kimazingira huku watu wakijipatia riziki.

Eneo hilo la Viwandani la utekelezaji wa mpango wa Climate WorX mtaani ni mfano wa kuunganisha hatua za kimazingira na uhusishaji wa jamii kuangazia miradi kama upanzi wa miti, matumizi ya kawi safi na usimamizi bora wa taka.

Katibu Omollo alihimiza jamii ya eneo hilo na wadau wengine kuhusika kikamilifu kwenye mipango kama hiyo kwani ina uwezo wa kutoa fursa za ajira na kuboresha hali ya maisha yao.

Omollo alisisitiza kujitolea kwa serikali kuunga mkono juhudi za mashinani za kuafikia maono ya taifa hili kwenye ruwaza ya mwaka 2030 na ajenda ya maendeleo endelevu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *