Katibu wa Idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni leo Jumatatu ameshiriki mkutano na wadau mbalimbali ili kuangazia suala la utapia mlo humu nchini.
Mkutano huo uliwaleta pamoja maafisa kutoka shirika la watoto la UNICEF na wawakilishi kutoka ubalozi wa Uingereza miongoni mwa wengine.
Hususan, mkutano huo ulilenga kutafuta njia za kukuza ushirikiano kwa kutoa kipaumbele kwa lishe katika juhudi za kuzuia magonjwa nchini.
“Majadiliano muhimu wakati wa mkutano huo yaliangazia changamoto za utapia mlo nchini Kenya na hatua zinazochukuliwa kwa sasa, ikiwa ni pamoja na usaidizi kutoka kwa Ofisi ya Jumuiya ya Kigeni na Maendeleo, FCDO na Hazina ya Lishe ya Watoto,” ilisema Wizara ya Afya katika taarifa.
Na huku Kenya ikilenga kuhakikisha upatkanaji wa afya kwa wote kupitia mipango ya utoaji huduma za afya ya msingi, wadau walisisitiza umuhimu wa lishe katika kuhakikisha ndoto ya Wakenya wote kupata huduma za afya kwa usawa inatimia.