Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni anasema serikali inafanya kila juhudi kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kutolewa kama kawaida katika hospitali za umma kote nchini.
Muthoni amesema miongoni mwa juhudi hizo ni kuendelea kufanya mazungumzo na Chama cha Madaktari nchini, KMPDU hasa kuhusiana na suala tata la malipo.
Akizungumza leo Alhamisi alasiri, Katibu huyo ametetea hatua ya serikali kutoa shilingi milioni 966 za kuwalipa madaktari wanagenzi.
Kulingana naye, hatua hiyo ilikuwa afueni kwa madaktari hao ambao walikuwa wamekaa kwa muda mrefu bila kulipwa.
Aidha, ameahidi kutii maagizo yatakayotolewa na mahakama kuhusiana na malipo hayo.
Kitita cha shilingi hizo milioni 966 kimepuuziliwa mbali na chama cha KMPDU kinachoilaumu serikali kwa kukiuka Mkataba wa Maelewano uliofikiwa miaka minane iliyopita.
KMPDU kinasema fedha hizo zinaashiria kila daktari mwanagenzi atakuwa akipokea shilingi elfu 70 kwa mwezi kabla ya makato, hatua inayokinzana na mkataba huo.
Chama hicho kimekuwa kikishinikiza kila daktari mwanagenzi alipwe shilingi 206,000 kwa mwezi kama ilvyokubaliwa kwenye mkataba wa mwaka 2017-2021.
KMPDU imetoa ilani ya siku 21 ya kufanya mgomo ikiwa serikali haitatimiza matakwa yake.
Ikiwa hilo litafanyika, huduma katika hospitali za umma zitaathirika pakubwa kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mgomo siku zilizopita.
Hadi kufikia sasa, madaktari wanagenzi wawili wamejitoa uhai kutokana na hali ngumu ya maisha iliyowasababishia msongo wa mawazo.