Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amemkubalia Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance, UDA Cleophas Malala awe akihudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri. Hatua hii ilipitishwa kwenye mkutano wa baraza hilo Jumanne, Juni 27, 2023.

Malala aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho yapata miezi minne iliyopita na sasa ameongezewa jukumu jingine.

Hata hivyo, Ikulu haikubainisha iwapo amefanywa kuwa Waziri asiye na wizara kama ilivyokuwa kwa Raphael Tuju, aliyehudumu kama Katibu Mkuu wa chama tawala kwa serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Wengine ambao wamekubaliwa kuhudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri ni washauri wa rais katika maswala mbalimbali ambao ni Monica Juma ambaye ni mshauri wa Rais katika maswala ya usalama, Mwenyekiti wa Baraza la Washauri wa Rais kuhusu Uchumi David Ndii na Bi. Harriette Chiggai ambaye ni mshauri wa rais kuhusu haki za wanawake.

Wanne hao walikula kiapo cha kudumisha siri leo katika Ikulu ya Nairobi kabla ya kuanza kwa mkutano wa Baraza la Mawaziri.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *