Mwanamuziki Kanye West amefuta akaunti yake ya mtandao wa X baada ya kuchapisha maneno kadhaa yanayoashiria chuki dhidi ya Wayahudi.
Awali, usimamizi wa mtandao wa X ulikuwa umeweka onyo la maudhui ya kutiliwa shaka kwenye akaunti hiyo ya Kanye.
Kanye alianza kuchapisha maneno hayo ya kusikitisha Ijumaa Februari 7, 2025 ambapo aliandika maneno kama vile kukiri kuwa mwanachama wa Nazi.
Aliandika pia kwamba haamini yeyote ambaye ni Myahudi na kwamba aliandika maneno hayo akiwa hajanywa pombe hata kidogo.
West aliyebadili jina na kuwa Ye mwaka 2022, aliendelea kuchapisha taarifa zisizo nzuri hatua iliyosababisha watu kadhaa kama vile David Schwimmer kumtaka mmiliki wa X Elon Musk kumpiga Ye marufuku.
Schwimmer alisema kwamba Ye amerejelea hulka yake ya mwaka 2022 akisema kwamba hawawezi kumkomesha kusema anayoyasema lakini wanaweza kumnyima jukwaa la kutoa maoni yake.
Alishangaa ni kwa nini Kanye West ambaye ana wafuasi milioni 32.7 kwenye mtandao wa X idadi ambayo ni mara mbili ya idadi jumla ya wayahudi anakwazwa na uwepo wao.
Schwimmer ambaye ni mwigizaji anasema matamshi ya Ye yanasababisha uhasama halisi dhidi ya wayahudi na hajui ni lipi baya zaidi kuliko lingine kati ya aliyoyachapisha Kanye.
West alianza kudhihirisha hulka ya kutopendelea wayahudi Disemba mwaka 2022 wakati alisema kwamba anampenda Hitler katika mahojiano na Alex Jones kwenye kipindi show Infowars.
Usemi wa Ye ulisababisha kampuni kadhaa zilizokuwa zikishirikiana naye kama vile Adidas, GAP na Balenciaga zikomeshe mikataba na yeye.