Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI Mohamed Amin leo Jumatano wanatarajiwa kufika mahakamani kuelezea kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kuipuuza mahakama.
Hii inafuatia agizo la mwezi jana kutoka kwa Jaji Diana Kavedza la kuwataka Kanja na Amin kuwapeleka mahakamani watu sita waliotekwa nyara mwezi Disemba, kufikia mwisho wa mwaka jana.
Kufuatia hatua ya Kanja na Amin kukosa kuwatoa watu hao sita, Jaji Bahati Mwamuye aliamuru kuwa wawili hao wafike mahakamani leo kujielezea ni kwa nini wasiadhibiwe kwa makosa ya kupuuza mahakama.
Kwenye kesi hiyo, wawili hao walishtakiwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kipchumba Murkomen.
Kesi hiyo iliwasilishwa na Tume ya Kutetea Haki za Kibinaadamu na chama cha mawakili nchini.
Kufikia sasa, ni watu watano pekee walioachiliwa: Ronny Kiplagat, Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli na Kelvin Muthoni huku Steve Mbisi akiwa bado hajapatikana.