Kanja matatani ‘kwa kuhudhuria mkutano wa kisiasa’

Martin Mwanje
2 Min Read
Douglas Kanja - Inspekta Mkuu wa Polisi

Chama cha Wanasheria nchini, LSK kimelaani vikali hatua ya Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kuhudhuria mkutano wa kisiasa ulioongozwa na Rais William Ruto katika eneo la Kieni, kaunti ya Nyeri jana Jumatano. 

Kwenye taarifa, Rais wa LSK Faith Odhiambo amesema kikatiba, Kanja anapaswa kuwahudumua Wakenya bila miegemeo yoyote ya kisiasa.

“Ushiriki na kauli za Inspekta Mkuu zinaibua mashaka makuu ya kitaasisi kwa Huduma ya Taifa ya Polisi, kwa sababu siyo tu kwamba zingeepukika bali pia hazikustahili,” alisema Odhiambo kwenye taarifa ya kurasa tatu aliyoitoa leo Alhamisi.

“Tangu mwanzo, tunapaswa kuelezea wazi kwamba Inspekta Mkuu ana wajibu wa kikatiba wa kuwahudumia Wakenya wote kwa usawa, bila kujali miegemeo ya kisiasa. Tuna mashaka ikiwa matukio ya jana Jumatano mjini Nyeri yalikuwa sarakasi za kisiasa, ambayo athari yake isiyokusudiwa inaweza kuwa kutenga watu fulani walio na maoni tofauti ya kisiasa na yale yaliyozungumzwa na Bw. Kanja kupitia uwepo na kauli zake kwenye mkutano wa jana.”

LSK inasema ikiwa hali kama hiyo itatokea, basi itakuwa ukiukaji mkubwa wa katiba.

Kulingana na chama hicho, hatua ya Kanja inakiuka kifungu cha 245(7) cha katiba, hali inayomweka katika hatari ya kubanduliwa madarakani.

Aidha, kinamtuhumu Inspekta Mkuu kwa kukosa kutoa kipaumbele kwa masuala muhimu yanayolikumba taifa kama vile utekaji nyara na badala yake kukimbilia kuhudhuria mikutano ya kisiasa.

Msemaji wa polisi Muchiri Nyaga amenukuliwa akikanusha madai kuwa Kanja alihudhuria na kuhutubia mkutano wa kisiasa huko Nyeri jana Jumatano.

 

Website |  + posts
Share This Article