Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Metropolitan la Nairobi, Philip Anyolo, amewataka viongozi wa kisiasa kupunguza hali ya joto la kisiasa inayoongezeka nchini.
Anyolo badala yake anawahimiza viongozi hao, kuzingatia utekelezaji wa ahadi zao za kampeni za mwaka 2022.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Yosefu Mlinzi huko Kamulu, Anyolo alikosoa wanasiasa kwa kujihusisha na matamshi ya kugawanya jamii wakati wa mikutano ya kandokando ya barabara.
Alisema kauli hizo haziakisi changamoto zinazowakabili Wakenya wa kawaida, hasa wale wanaoishi katika umaskini na familia zilizokoseshwa makazi kutokana na mafuriko.
Askofu huyo Mkuu aliwataka viongozi kuiga maadili ya Mtakatifu Yosefu, akiwahimiza kuwatendea wengine kwa haki na heshima.
Alionya kuwa mivutano ya kisiasa inayoendelea haichangii kujenga uchumi wa nchi, bali inasababisha upotoshaji wa juhudi za utoaji huduma kwa wananchi.
Wakati huo huo, Anyolo aliwahimiza waumini wa Kanisa Katoliki kuwachagua viongozi wenye uadilifu katika chaguzi zinazoendelea za kanisa na makundi ndani ya Jimbo Kuu, akisisitiza umuhimu wa uongozi unaoongozwa na imani na maadili mema.