Kanisa la Anglikana nchini Uganda limetangaza marufuku dhidi ya uwekaji wa maua juu ya jeneza na juu ya kaburi katika hafla za mazishi.
Badala yake, kanisa hilo litaangazia upanzi wa miche ya miti kwenye hafla hizo.
Kulingana na viongozi wa kanisa hilo, miti itasaidia pakubwa katika kuweka kumbukumbu za wafu huku ikitunza mazingira, ikilinganishwa na maua yanayonyauka haraka.
Hatua hii inawiana na mkakati mpya wakanisa Anglikana la Uganda mpango unaoangazia uimarishaji wa shughuli za utunzaji wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Tangazo la marufuku ya maua kwenye mazishi lilitolewa wakati wa uzinduzi wa mpango wa kimkakati wa kanisa hilo wa mwaka 2026 hadi 2031 katika eneo la Masaka.
Hafla hiyo iliongozwa na askofu mkuu Stephen Kaziimba Mugalu.
Mpango huo wa kimkakati utaongoza shughuli za kanisa Anglikana nchini Uganda kwa miaka mitano na maudhui yake ni “Kuhamasisha wakristo kwa maendeleo ya kijumla”.
Dkt. Julian Bagyendera ambaye alisaidia katika kuandaa mpango huo alifichua kwamba kutupiliwa mbali kwa tamaduni ya kuweka maua katika mazishi ni sehemu ya maazimio ya mpango huo.
Azimio husika ni kuimarisha utunzaji wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunasema kwamba tunaweza kuhimiza upanzi wa miche ya miti badala ya kuleta maua ambayo huenda yakaathiri mazingira kwani mengine ni bandia.” alisema Julian.