Kanisa katoliki limetoa wito wa kukataliwa kwa michango ya fedha ya kisiasa, kama njia moja ya kudumisha hadhi ya makanisa hapa nchini.
Kupitia kwa taarifa, Baraza la Maaskofu wa kanisa Katoliki KCCB, lilitoa wito wa kutekelezwa kwa maadili kwa kukatalia mbali fedha za wanasiasa, ambazo henda zikahujumu uhuru na kanisa hapa nchini.
Wakati huo huo, Maaskofu huo waliwataka wanasiasa kujiepusha na kutumia majukwa ya kanisa kuendeleza kampeini zao za kisiasa.
“Viongozi wa kisiasa wanahimizwa kudhihirisha maadili, kwa kushughulikia maswala yaliyoibuliwa na KCCB, ikiwa ni pamoja na ufisadi, ukiukaji wa haki za kibinadamu, mizozo ya kisiasa na ahadi zisizotimizwa,” walisema Maaskofu hao.
Aidha waliitaka kanisa kutoegemea upande wowote, bila ushawishi wowote wa kisiasa, ili kutoa huduma bora za kidini kwa jamii.
Maaskofu wa hao wa kikatoliki hata hivyo waliwakaribisha wanasiasa kuhudhuria ibada kama waumini wengine wa kawaida bila ya kujaribu kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
Akizungumza mjini Embu juma lililopita, Rais William Ruto alitoa ahadi ya kushughulikia kikamilifu maswala yote yaliyoibuliwa na kanisa katoliki.