Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen, amepongeza kampuni ya ndege ya Skyward Express kwa kuzindua safari za ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi jijini Mombasa.
Murkomen alitaja hatua hiyo kuwa itakayoimarisha uunganishaji wa kitaifa na ule wa kimataifa, na hivyo kupiga jeki biashara, usafiri na ukuaji wa uchumi pamoja na kutoa nafasi za ajira.
Akizungumza katika uwanja wa ndege wa Moi jijini Mombasa baada ya kutua kwa ndege ya kwanza ya kampuni hiyo kutoka uwanja wa JKIA, Waziri huyo alidokeza kuwa kutokana na sera mpya kuhusu uchukuzi wa angani, serikali itahakikisha kampuni nyingi zinapata fursa ya biashara hapa nchini.
“Tumegundua kwamba wengi wangependa kushuhudia kampuni nyingi za kigeni zikifanya biashara hapa nchini, na tumefungua huo mlango ili kusaidia utalii wa nyumbani. Aidha, tutatekeleza hayo kwa makini kuhakikisha hatutatizi kampuni za hapa nyumbani,” alisema Murkomen.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa kampuni ya Skyward Express Mohammed Abdi alielezea shukrani zake kutokana na msaada ambao kampuni yake imepokea kutoka kwa serikali, mawakala wa usafiri pamoja na wateja.
“Usafiri kati ya Mombasa na Nairobi utaendelea kuwa muhimu. Kwa muda wa miaka saba, kampuni ya Skyward imekuwa ikihudumu kati ya uwanja wa ndege wa Wilson na Mombasa, na itaendelea kuwekeza katika safari hiyo,” alisema Abdi.
Aliongeza kuwa kutokana na huduma zake mpya, kampuni hiyo hivi karibuni itafupisha muda wa safari kati ya Mombasa na Nairobi.