Serikali imemulika kampuni 16 zinazohusika na utoaji wa ajira katika nchi za nje kwa kuhudumu bila leseni hitajika.
Haya yanajiri wakati ambapo visa vya ulaghai kuhusu ajira ughaibuni vinazidi kuongezeka huku katibu wa leba na ujuzi Shadrack Mwadime akisema kampuni hizo zinachunguzwa.
Wizara ya leba ilishirikiana na idara ya upelelezi wa jinai DCI kutambua kampuni hizo na inahimiza wanaotafuta ajira kuchunguza kampuni wanazotumia ili kuepuka kulaghaiwa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Mwadime alijuza wakenya kwamba kila tangazo la ajira ughaibuni au stakabadhi za mahitaji ya kupata ajira ughaibuni ni lazima viwe vimeidhinishwa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya kitaifa ya ajira.
Taarifa ya Mwadime imetolewa wakati ambapo kashfa nyingine imebainika jijini Eldoret ambapo watu wapatao 300 wanadaiwa kulaghaiwa hela baada ya kuahidiwa nafasi za ajira nchini Canada.
Kila mmoja wao anasemekana kutoa shilingi elfu 300 hadi elfu 350 za kutayarisha Visa na stakabadhi nyingine zinazohitajika kwa usafiri wao.
Gavana wa kaunti ya Uasin Gishu Jonathan Bii tayari ameagiza uchunguzi kuhusu wahusika wa kashfa hiyo akisema wamesababisha jiji hilo jipya kuwa na sifa mbaya.
Kulingana na Mwadime uhalali wa wanaotoa ajira ughaibuni unaweza kuthibitishwa kupitia tovuti ya mamlaka ya kitaifa ya ajira ambayo ni NEAIMS.GO.KE.
Katika tovuti hiyo pia kuna orodha ya kampuni halali za utoaji wa ajira ughaibuni.