Kambua apaaza sauti kuhusu mauaji ya wanawake nchini

Marion Bosire
1 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya Kambua Mutsembi Manundu ambaye wengi wanamfahamu kwa jina lake la kwanza amepaaza sauti kuhusu mauaji ya wanawake humu nchini.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya polisi kutoa takwimu zinazoonyesha kwamba wanawake wapatao 97 wameuawa katika muda wa siku tisini humu nchini.

Kambua anakumbuka jinsi shangazi yake na binti yake waliuawa nyumbani kwao huko Mtopanga kaunti ya Mombasa mwaka 2013, na kama familia hawajawahi kupata haki na hiyo kesi iliisha.

“Siwezi kusahau jinsi nyumba yao ilikuwa siku hiyo na mwonekano wa miili yao.” alikumbuka Kambua huku akitaja matukio ya mwaka 2024.

Anasema kwamba mwanamke mmoja amekuwa akiuawa kinyama kila siku katika kipindi cha miezi mitatu, takwimu ambazo anasema zinafaa kuchukiza wakenya ili wachukue hatua.

“Mhamiaji haramu, aliyeua mke wake na watoto nchini Ethiopia na kukimbilia Kenya ameua wanawake wanne tunaofahamu katika kipindi cha chini ya siku 30.” aliandika Kambua kwenye Instagram.

Aliendelea kusema kwamba mshukiwa huyo, alichemsha mwili wa mwathiriwa wake wa mwisho akishangaa jinsi maafisa wa upelelezi wa jinai wanadai kwamba mauaji hayo sio ya kijinsia.

“Ninaweza hata kulia.” alimalizia mwimbaji huyo huku akisema kwamba maisha ya wanawake ni muhimu na kuhimiza kukomeshwa kwa mauaji yao.

Share This Article