Ni afueni kwa kambi ya wakimbizi ya ZamZam nchini Sudan, baada ya kupokea shehena ya kwanza ya msaada, kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Kambi hiyo ambayo imewahifadhi wakimbizi 500,000, imekosa kupokea misaada kwa kipindi cha miezi kadhaa kutokana na mapigano makali na barabara mbovu iliyosababishwa na mvua.
Malori ya umoja wa mataifa yaliwasili Ijumaa, katika kambi hiyo, ambako maelfu ya wakimbizi wametafuta hifadhi kufuatia vita vya miezi 18 nchini Sudan.
Vita vya Sudan vimesababisha hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani ambako takribani watu milioni 10 walilazimika kuhama makazi yao.
Idadi ya watu katika kambi ya Zamzam imeongezeka tangu mwezi Aprili wakati wapiganaji walipoanza kukabiliana na majeshi ya serikali kutwaa mji wa el-Fasher.
El-Fasher ndio mji pekee unaodhibitiwa na majeshi ya serikali katika eneo la Darfur.