Kamati ya uwiano ya bunge kuandaa mikutano ya amani

Mikutano hiyo itapiga jeki juhudi za serikali za kuhakikisha amani katika maeneo husika.

Marion Bosire
1 Min Read
Adan Yusuf Haji, mwenyekiti, kamati ya bunge kuhusu uwiano na fursa sawa

Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Uwiano na Fursa Sawa imeanzisha mpango wa kuandaa mikutano ya amani katika maeneo ambayo hukumbwa na vurugu kila mara kwa nia ya kuzitokomeza.

Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti Adan Yusuf Haji ambaye ni mbunge wa Mandera Magharibi, iliandaa majadiliano kuhusu mikutano hiyo itakayoandaliwa katika kaunti nne zilizotambuliwa kama zinazokumbwa na vurugu kila mara.

Vurugu hizo husababishwa na hatua ya kung’ang’ania raslimali, uchochezi na uongozi wa kisiasa miongoni mwa sababu nyingine.

Kaunti zilizotambuliwa ni Malindi, Kilifi, Lamu na Baringo.

Haji alisema kamati hiyo inafurahikia juhudi za serikali za kukomesha vurugu na kurejesha amani katika maeneo husika.

Alifafanua kwamba kama kamati wanataka kupiga jeki juhudi hizo za serikali kupitia mikutano ya amani.

Kulingana naye, mipango hiyo inawiiana na jukumu la kamati hiyo ya bunge la kuhakikisha utangamano wa jamii mbali mbali na kuishi pamoja kwa amani.

Mwenyekiti huyo alisema kamati hiyo itatekeleza mipango hiyo ya mikutano ya amani kwa ushirikiano na kamati za usalama za maeneo husika zikiongozwa na makamishna wa kaunti.

Mikutano hiyo itahusisha jamii zinazozozana, viongozi wa maeneo husika, viongozi wa kidini na wadau wengine ambao ni muhimu kwa juhudi za kuhakikisha amani.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *