Wenyeviti wenza wa kamati inayoongoza mazungumzo baina ya serikali na upinzani, wamepuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa migawanyiko katika mazungumzo hayo kutokana na matakwa mapya kutoka kwa muungano wa Azimio la Umoja one Kenya.
Muungano huo wa upinzani umehoji matukio ambayo yamekuwa yakitokea hivi maajuzi yakiwemo madai ya kutekwa nyara kwa aliyekuwa kiongozi wa kundi la Mungiki Maina Njenga na pia ukaishtumu serikali kwa kuwaondoa maafisa wa usalama wanaowalinda baadhi ya viongozi wa upinzani.
Wanachama wa kamati hiyo ya mazungumzo walifanya mkutano wa faraghani kwa takriban saa tatu.
Hata hivyo kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ambaye anaongoza ujumbe wa upinzani amepuuzilia mbali madai ya kutokota kwa mzozo wa kisiasa katika mazungumzo hayo.
Kiongozi wa walio wengi bungeni Kimani Ichung’wah pia alipuuzilia mbali madai ya kuwepo kutoelewana baina ya wanachama.
Haya yanawadia huku kundi hilo likitarajiwa kuanza mazungumzo kuhusu ajenda tano zilizoafikiwa.
Serikali imeelezea kusita kuitikia matakwa ya kukagua matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita.
Muungano wa Azimio unataka sheria ya fedha ya mwaka 2023 kutupiliwa mbali ili kuwezesha pande hizo mbili kukubaliana namna ya kuwanasua wakenya kutoka kwa gharama ya juu ya maisha, na kuchunguza upya ushuru mbalimbali unaotozwa.
Kamati hiyo ya wanachama kumi inaendelea kupokea nyaraka za maoni kutoka kwa wananchi.