Kamati ya kuthibitisha madeni yanayodaiwa NHIF yazinduliwa

Uzinduzi uliongozwa na waziri wa Afya Aden Duale na lengo kuu la kubuni kamati hiyo ni kuhakiki malipo ambayo NHIF haikuwa imetoa kwa vituo vya afya kufikia wakati wa kufutiliwa mbali ya jumla ya bilioni 33.

Marion Bosire
2 Min Read

Wizara ya Afya imezindua rasmi kamati iliyobuniwa ili kudhibitisha madeni ambayo yanadaiwa iliyokuwa bima ya kitaifa ya afya NHIF, katika hatua ya kushughulikia madeni hayo.

Shughuli ya uzinduzi iliongozwa na waziri wa Afya na lengo kuu la kubuni kamati hiyo ni kuhakiki malipo ambayo NHIF haikuwa imetoa kwa vituo mbali mbali vya afya kufikia wakati wa kufutiliwa mbali ya jumla ya bilioni 33.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa James Masiero Ojee, na Dkt. Anne Wamai kama naibu mwenyekiti imejukumiwa kutathmini uhalisia wa madeni hayo.

Kazi ya kamati hiyo itahakikisha uwazi, uwajibikaji na thamani ya pesa katika mfumo wa Afya nchini. Wanachama watahitajika kutambua madai ya ulaghai, uwongo na yaliyopitiliza, kupendekeza mabadiliko na namna ya kushughulikia madeni hayo.

Waziri Duale alisisitiza kwamba serikali tayari imelipa madeni yaliyokuwa chini ya shilingi milioni 10, kufuatia maelekezo ya Rais William Ruto.

Hospitali zilizokuwa na mkataba na NHIF na ambazo madeni yao yalikuwa chini ya shilingi milioni 10 zilikuwa asilimia 91 ya hospitali zote zilizokuwa zikishirikiana na NHIF.

Hospitali zinazodai malipo ya zaidi ya shilingi milioni 10 sharti zipitie mpango wa uthibitishaji ambao unatarajiwa kukamilika katika muda wa siku 90.

Masuala yatakayoangaziwa ni pamoja na hospitali zilizotuma maombi ya malipo bila mkataba faafu, malipo yaliyozidishwa, madai ya malipo ya upasuaji ambao haukufanyika na madai yaliyorudiwa zaidi ya mara moja ili kuhakikisha ni madai halali pekee yanalipwa.

Duale alidhihirisha imani katika uwezo wa kamati hiyo kurejesha imani ya umma na kuimarisha uadilifu katika mfumo wa afya humu nchini.

Aliwataka wadau wote waunge mkono mpango huo.

Website |  + posts
Share This Article