Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, ameagiza kamati ya bunge kuhusu Usalama na Utawala, kuwasilisha uchunguzi wa awali kuhusu kifo cha Albert Ojwang’.
Ripoti hiyo ambayo inatarajiwa kuwasilishwa Alhamisi alasiri, inatarajiwa kuifahamisha bunge kuhusu hatua za zilizopigwa za uchunguzi wa kifo cha Albert Ojwang.
Agizo la Wetang’ula lilijiri kufuatia wasiwasi ulioibuliwa na wabunge, wakiongozwa na mbunge wa Nyando Jared Okello, aliyetaja swala hilo kuwa la dharura.
“Ninafahamu kuwa siku ya Alhamisi ni siku ya kusomwa kwa bajeti, lakini tutakuwa na saa moja na nusu kabla ya shughuli ya bajeti kuanza. utawasilisha uchunguzi wa awali Alhamisi kufahamisha bunge na taifa kuhusu hatua za uchunguzi zilizochukuliwa hadi sasa,’ alisema Spika Wetang’ula.
Aliwahakikishia wabunge kwamba watakuwa na fursa ya kuchangia punde tu taarifa hiyo itawasilishwa bungeni.
Mwenyekiti wa kamati ya Usalama wa Taifa na Utawala Gabriel Tongoyo, alikiri kuwa swala hilo ni la dharura sio tu kwa bunge, lakini kwa taifa nzima kwa jumla.