Kamati ya bunge yataka orodha ya waliokwepa kulipa mikopo ya Hustler

Dismas Otuke
1 Min Read

Kamati ya bunge la kitaifa imeamrisha wasimamizi wa Hazina ya Hustler kuwasilisha orodha ya wateja ambao wamekataa kulipa mikopo waliyochukua.

Orodha hiyo itajumuisha majina, nambari za simu za waliokataa kulipa mikopo hiyo, maeneo bunge yao na kiwango cha pesa walichokopa.

Haya yanajiri baada ya hazina hiyo kufichua kuwa asilimia 78 ya shilingi bilioni 13 zilizotolewa hazijarejeshwa na waliokopa.

Kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Migori Fatuma Zainab ilikuwa ikimhoji Katibu wa Biashara Ndogo na Kati Susan Mang’eni na kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Hazina ya Hustler Elizabeth Nkukuu walipofika mbele yake kujibu maswali ya wabunge kuhusu matumizi ya pesa ilizotengewa hazina hiyo.

Hata hivyo, mkutano huo wa kukagua matumizi ya fedha haukukamilika baada ya wasimamizi wa hazina hiyo kushindwa kutoa stakabadhi za matumizi 19.

Wabunge wamehoji kukosekana kwa wataalam wa kusimamia hazina hiyo na kutilia shaka jinsi shilingi bilioni 13 zilivyotolewa kama mikopo bila wafanyakazi wa kutosha.

Pia wasimamizi walifichua kuwa hazina hiyo haina bima wala maafisa wa kufuatilia mikopo.

TAGGED:
Share This Article