Juhudi za kutafuta suluhu ya mizozo ya ardhi katika kaunti ya Kilifi zimechacha huku kamati ya bunge la taifa ya kushughulikia malalamishi ya umma ikifika kaunti hiyo kusikiliza vilio vya wakazi zaidi ya 30,000 ambao wameishi kama maskwota kwa zaidi ya miaka arobaini.
Kamati hiyo ikiongozwa na mbunge wa Kitui Mashariki Nimrodi Mbai iko mbioni kushughulikia malalamishi ya umma eneo hilo kuhusu kucheleweshwa kwa uamuzi wa kurudisha umiliki wa ardhi kwa wakazi ambao wamesumbuliwa na wanyakuzi wa ardhi bila kupata usaidizi wowote.
Wakiambatana na mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya ambaye ndiye aliyewasilisha malalamishi ya umma kwa bunge la kitaifa, wabunge hao waliambia vyombo vya habari kwamba watafanya kila juhudi ikiwemo kuundwa kwa sheria zitakazorahisisha mchakato wa kusuluhisha matatizo ya umiliki wa ardhi.
Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo, huenda wakaazi wanaoishi maeneo ya Mnarani, Kibarani na Tezo wakapata afueni kubwa baada ya kuahidiwa kupata suluhu ndani ya miezi mitatu.
Mamia ya wakazi walioathirika na mizozo ya ardhi walijitokeza kuzungumza na wabunge hao huku wakiwa na matumaini ya kupata hatimiliki zao za ardhi hivi karibuni ili waishi kwa amani.
Visa vya unyakuzi wa ardhi mjini Kilifi vimekithiri huku maelfu ya wakazi wakiishi na hofu ya kufurushwa kwa kushindwa kupata hatimiliki zao.
Hali hiyo imesababisha wakazi wengi kujipata pabaya kufuatia kubomolewa kwa makazi yao na kufurushwa kutoka kwenye ardhi ambamo wameishi kwa miaka mingi.
Taarifa ya KNA Kilifi