Kamati ya bunge la taifa kuhusu ulinzi, ujasusi na Mambo ya Nje, leo ilizuru taasisi kadhaa zinazoendeshwa na vikosi vya ulinzi katika kaunti ya Uasin Gishu.
Ikiongozwa na mbunge wa Kajiado ya Kati Memusi Kanchory, kamati hiyo ilishiriki mazungumzo na Meja Jenerali George Okumu, Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza risasi na zana zingine za kijeshi, Brigedia John Kipya, Kamanda wa chuo cha mafunzo ya kijeshi na Kanali K. Masai, Kamanda wa hospitali ya level 4 ya Eldoret.
Wabunge hao waliridhishwa na hospitali hiyo ya kisasa ya Level 4 iliyo na vitanda 150.
Baadhi ya huduma zinazopatikana katika hospitali hiyo ambayo ilianza kutoa huduma mwaka 2022, ni pamoja na matibabu ambapo wagonjwa huruhusiwa kurejea nyumbani, wagonjwa kulazwa na kujifungua kwa kina mama.
Kamanda wa hospitali hiyo Kanali Col. K. Masai, aliambia kamati hiyo kwamba, hospitali hiyo inalenga kuanzisha matibabu ya kuchomeka na huduma za Onkolojia.
Vile vile, kamati hiyo ilizuru kiwanda cha kutengeneza risasi na zana zingine za kijeshi (KOFC).
“Kiwanda hichi hakisaidii tu katika usalama wa taifa, lakini pia huchangia katika ukuaji wa uchumi wa ndani,” alisema Fred Ikana mbunge wa Shinyalu.
Kamati hiyo pia ilizuru chuo cha kutoa mafunzo ya kijeshi kilicho katika kambi ya kijeshi ya Moi mjini Eldoret, ambayo ina uwezo wa kutoa mafunzo kwa wanajeshi 5,500.
Wabunge hao walitoa ahadi ya kuendelea kuunga mkono vikosi vya ulinzi nchini, KDF.