Kamati ya bunge kuhusu habari yajadili changamoto za kiteknolojia nchini

Tom Mathinji
2 Min Read

Kamati ya bunge kuhusu Mawasiliano, Habari na Ubunifu inayoongozwa na mbunge wa Dagoretti kusini John Kiarie, inashiriki mkutano ulioandaliwa na kampuni ya kutoa huduma za kiteknolojia hapa nchini  (TESPOK), kujadili sera za kimataifa na changamoto zinazokabili teknolojia, ulinzi wa deta, usalama wa mtandaoni na akili mnemba.

Kamati hiyo inatumia warsha hiyo kufahamu mbinu bora za kimataifa za kiteknolojia, pamoja na kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau tofauti.

Akizungumza katika mkutano huo, Kiarie alitoa wito wa kutekelezwa kwa sera zinazowiana na viwango vya kimataifa.

“Tunalenga kuziba pengo la kisheria na kupeleka mbele sekta hii,” alisema Kiarie.

Afisa Mkuu mtendaji wa kamuni ya  KICTANet, alielezea ufanisi ulioafikiwa kuhusu ulinzi wa deta tangu sheria ya ulinzi wa deta ilipoanzishwa hapa nchini miaka mitano iliyopita, huku akitoa mapendekezo ya kuimarisha zaidi ulinzi wa deta na kupiga jeki uchumi wa deta.

Fiona Asonga, afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya TESPOK, alishinikiza kutekelezwa kwa sheria ya habari na mawasiliano KICA, na ile ya KICA mwaka 2024, ili kuwezesha sekta hiyo kukabiliana na maswala ibuka ya kiteknolojia.

kwa upande wake, mtaalam wa kampuni ya Huawei Adam Lane, alizungumzia sera za uchumi wa dijitali duniani na jinsi taifa hili linaweza faidika na mchango wa sekta ya ICT.

Lane alisema manufaa hayo yanaweza afikiwa kupitia utoaji mafunzo, upatikanaji wa deta kwa shughuli za utafiti na ukuzaji wa programu na suluhisho zitokanazo na akili mnemba miongoni mwa mengine.

Kamati hiyo ilikubaliana kuhusu haja ya kuwa na ushirikiano wa asasi mbali mbali, ili kuimarisha usalama wa mtandaoni na kubuni sekta imara ya kibinafsi kuwahudumia wakenya vilivyo.

TAGGED:
Share This Article