Kamanda mkuu wa Hamas auawa Gaza

Hamas ilithibitisha Jumapili kwamba Samir Abu Younis, aliuawa katika shambulizi huko al-Mawasi, Khan Younis, Jumamosi.

Marion Bosire
2 Min Read

Kamanda mkuu wa kundi la Hamas ameuawa katika shambulizi la ndege isiyo na rubani la Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza, licha ya uwepo wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza Oktoba 11, 2025.

Hamas ilithibitisha Jumapili kwamba Samir Abu Younis, aliyekuwa kamanda wa kikosi chake cha Rafah, aliuawa katika shambulizi lililolenga eneo la al-Mawasi, Khan Younis, Jumamosi.

Jeshi la Israel na shirika lake la usalama la Shin Bet zilikuwa zimetangaza awali kuwa zilitekeleza shambulizi la ndege isiyo na rubani dhidi ya kamanda mkuu wa kijeshi wa Hamas katika eneo hilo.

Shambulizi hilo pia liligonga hema iliyokuwa ikiwahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao, na kujeruhi watu wengine wawili.

Majeruhi hao walipelekwa katika Hospitali ya Nasser Medical Complex kwa matibabu, kwa mujibu wa wahudumu wa afya.

Eneo la al-Mawasi, lililotajwa awali na Israel kuwa eneo la kibinadamu, lina maelfu ya Wapalestina waliolazimika kuishi kwenye mahema baada ya kuhama makazi yao.

Wizara ya Afya ya Gaza iliripoti kwamba mashambulizi ya Israel yaliua watu 16 na kujeruhi wengine 68 katika muda wa saa 48 ulioishia Jumamosi.

Tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaanze kutekelezwa Oktoba 11, 2025, Wapalestina wasiopungua 1,643 wameuawa na wengine 5,964 kujeruhiwa. Miili ya watu 850 pia imetolewa chini ya vifusi.

Kwa jumla, wizara hiyo inasema watu 74,695 wameuawa na 176,093 kujeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha vita Gaza Oktoba 2023.

Share This Article