Viongozi wa baadhi ya vyama tanzu vya muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya wameapa kuendelea kusimama na Wakenya.
Wanashikilia kwamba kamwe hawatajiunga na serikali ya Kenya Kwanza.
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Eugine Wamalwa wa DAP-K na Jeremiah Kioni wa Jubilee, walikuwa wakizungumza katika kanisa moja mjini Thika, kaunti ya Kiambu jana Jumapili.
Walikikosoa chama cha ODM kwa kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza wakitaja hatua hiyo kuwa ya kuwasaliti Wakenya.
Hii ni baada ya wanachama wanne wa chama hicho kuteuliwa kuhudumu kama mawaziri kwenye serikali ya Rais William Ruto.
Watatu hao walisema pia kwamba watazindua vuguvugu kwa jina “Okoa Kenya” na watamuunga mkono Kalonzo Musyoka kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Walihimiza vijana wa Kenya watume maombi ya vitambulisho vya kitaifa na wajisajili kuwa wapiga kura kama njia ya kujiandaa kubadilisha nchi kupitia uchaguzi.