Kalonzo na Eugene wasema upinzani utasalia imara bila Raila

Martin Mwanje
1 Min Read

Muungano wa Azimio utasalia imara hata ikiwa Raila Odinga atachaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC. 

Hii ni kwa mujibu wa kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.

Kalonzo aliunga mkono matamshi ya Raila kwamba hata akichaguliwa kwenye wadhifa huo, bado anaweza kuendelea na majukumu yake kwani afisi yake itakuwa nchini Ethiopia na usafiri wa ndege ni wa saa mbili pekee kutoka hapa nchini.

Hata hivyo, Naibu Rais huyo wa zamani, aliongeza kuwa yuko tayari kuvalia njuga majukumu ya Raila iwapo atalazimika kufanya hivyo.

Kalonzo ambaye aliandamana na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa, aliwahimiza wanafunzi kutoka shule mbalimbali za upili waliohudhuria warsha hiyo, kutia bidii masomoni kwa faida ya maisha ya halafu.

Kwa upande wake, Wamalwa alisema nchi hii inahitaji taasisi imara kwa faida ya Wakenya wote, hivyo kuondoka kwa Raila kusiwatie wananchi kiwewe.

Warsha hiyo ya juma moja, imeleta pamoja washikadau wengi wanaolea demokrasia nchini hasa vyama vya kisiasa.

Viongozi wengi wa kisiasa wamehudhuria warsha hiyo huku wengine zaidi wakitarajiwa kuhudhuria warsha hiyo itakayotamatika kesho Jumamosi.

Share This Article