Kalonzo ataka mchakato wa kuunda upya IEBC kuharakishwa

Martin Mwanje
2 Min Read
Kalonzo Musyoka - Kiongozi wa chama cha Wiper

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amelalamikia kucheleweshwa kwa mchakato wa kuunda upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC. 

Akiwahutubia wanahabari leo Jumanne, Kalonzo amesema hatua hiyo imelemaza mno utendakazi wa IEBC.

“Hata baada ya Mswada wa (Marekebisho) ya IEBC 2023 – moja ya miswada muhimu ya kisheria ya NADCO – kutiwa saini kuwa sheria, bado hatuna tume ya kutekeleza maboresho ya uchaguzi. Nia njema ya kisiasa inakosekana, uingiliaji wa taasisi umewazuia Wakenya dhidi ya kuwa na tume kamili ya IEBC inayofanya kazi,” alidai Kalonzo.

“Kwa zaidi ya mwaka mmoja, IEBC haijakuwa na makamishna. Hii imekuwa na athari kubwa kwa utekelezaji wa shughuli kadhaa za tume hiyo kama vile kusimamia chaguzi ndogo, ugavi wa mipaka na uchambuzi wa sera kadhaa.

Kalonzo sasa anazitaka pande zote husika ikiwa ni pamoja na vyama vya kisiasa, mashirika ya kijamii na taasisi za serikali kuungana na kuunga mkono mapendekezo yaliyomo katika Ripoti ya Kamati ya Uwiano wa Kitaifa (NADCO).

Kiongozi huyo wa Wiper pia ametaja ucheleweshaji wa utoaji wa vitambulisho vya kitaifa, michakato ya urasimu, ufisadi, uitishaji rushwa na ugumu wa wakazi katika sehemu za vijijini kufika katika vituo vya kutuma maombi ya kupatiwa vitambulisho vya kitaifa kuwa changamoto zinazowazuia Wakenya wengi kujiandikisha kama wapiga kura.

“Changamoto hizi, ikiwa hazitasuluhishwa, zitasababisha idadi ndogo ya Wakenya kujitokeza kupiga kura na hivyo kuwanyima Wakenya wengi haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.”

Kalonzo sasa anatoa wito wa changamoto hizo kuangaziwa mara moja.

 

Share This Article