Bingwa mtetezi wa dunia wa mashindano ya WRC Kalle Rovanpera wa Toyota Gazoo amesajili ushindi wake wa pili katika mkondo wa tatu wa msimu uliokamilika Jumapili jioni katika kituo cha Hells Gate Power Stage.
Raia huyo wa Finland akielekezwa na Jonne Halttunen, alijipatia uongozi wa zaidi ya dakika moja baada ya kushinda vituo vyote sita vilivyojaa mawe siku ya Ijumaa karibu na Ziwa Naivasha, na kudumisha uongozi huo Jumamosi na Jumapili licha ya kutoshinda kituo chochte cha mashindano.
Dereva huyo mwenye umri wa miaka 23 alizoa pointi 20 katika mashindano ya Safari Rally na kutawazwa bingwa kwa muda wa saa 3, dakika 36 na sekunde 4, akimwacha mwenzake wa Toyota Katsuta Takamoto kwa dakika 1 sekunde 37.8 huku Adrien Fourmaux wa Ford akichukua nafasi ya tatu.
Carl Tundo, akielekezwa na Tim Jessop, alikuwa dereva bora wa humu nchini akichukua nafasi ya saba katika kitengo cha WRC 2 na wa 16 kwa jumla.
Makala ya 71 ya mashindano ya Safari Rally, ambayo yalirejea wakati wa msimu wa Pasaka kwa mara ya kwanza baada ya miaka 26, yaliwavutia madereva 26 walioshindana katika umbali wa kilomita 376.1 uliogawanywa kwa vituo 19.
Mwingereza Gus Greensmith aliibuka mshindi wa kitengo cha WRC2 akifuatwa na Mswidi Oliver Solsberg huku Kajetan Kajetoniwicz wa Poland akimaliza wa tatu.
Mashindano ya WRC yataelekea Zagreb, Croatia kwa mkondo wa nne kati ya tarehe 18 na 21 mwezi ujao.