Kaka wawili Jamil Longton na Aslam Longton, waliotekwa nyara na watu wasiojulikana mwezi mmoja uliopita, wamepatikana wakiwa hai mtaani Gachie, kaunti ya Kiambu.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Rais wa Chama cha Mawakili nchini, LSK Faith Odhiambo.
Kupitia ukurasa wake wa X, wawili hao wamepatikana mapema leo Ijumaa huku hatima ya mshirikishi wa vuguvugu la Free Kenya Bob Njagi, ambaye walitekwa nyara pamoja, ikiwa haijulikani.
Watatu hao walitoweka kutoka Kitengela Agosti 19 baada ya kutekwa nyara na watu walioaminika kuwa polisi, ingawa idara hiyo ilikanusha kufahamu waliko na kutojihusisha na utekaji nyara huo.
LSK kwenye kesi iliyowasilisha mahakamani iliwataka polisi kuwaachilia huru watatu hao na kufichua waliko.
Kisa hicho kilisababisha Kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi wakati huo Gilbert Masengeli kuhukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kwa kukosa kufika mahakamani mara tatu kuelezea waliko watu hao waliotekwa nyara.