Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe, ametoa wito kwa wabunge kubuni sheria zilizo na adhabu kali dhidi ya wale wanaojihusisha na mbegu na mbolea ghushi, akitaja uovu huo kuwa ni hatari kwa utoshelevu wa chakula hapa nchini.
Kagwe alisema sekta ya kilimo ni muhimu katika ukuaji wa kiuchumi na kijamii, kupitia utoaji fursa za ajira, kuimarisha utoshelevu wa chakula na ubadilishanaji wa sarafu za kigeni.
“Mbegu na mbolea bandia zinahatarisha utoshelevu wa chakula hapa nchini, na hatuwezi waruhusu walaghai kuwahujumu wakulima wetu,” alisema waziri Kagwe.
“Ninawasihi wabunge, wakati wa kubuni sheria kali ni sasa. Tunahitaji sheria zilizo na adhabu kali kwa wale wanaojihusisha na bidhaa hizo ghushi ambazo ni hatari,” aliongeza waziri huyo.
Waziri huyo aliyasema hayo leo Ijumaa alipowasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka 2025 kwa kamati ya bunge la taifa kuhusu kilimo na ustawi wa mifugo inayoongozwa na Dkt. John Mutunga.
Kwenye kikao hicho, waziri Kagwe alisifu sheria kuhusu sukari ya mwaka 2024, aliyosema imezaa matunda kwani uzalishaji sukari hapa nchini umeongezeka hadi metrik tani 820,000 mwaka 2024.
“Ninahakika kwamba ifikapo mwaka 2026, Kenya itauza sukari yake katika masoko ya ng’ambo,” alidokeza waziri huyo.
Aidha alipigia debe kampeni inayoendelea ya kuwachanja mifugo kote nchini, akisema hatua hiyo itafanikisha kutokomeza ugonjwa wa Miguu na Midomo(FMD) na ule wa Peste des Petits Ruminants (PPR) na hivyo kuhakikisha mifugo walio na afya.
“Magonjwa hayo hayahujumu tu uzalishaji katika sekta ya mifugo, lakini pia husababisha taifa hili kupata hasara ya kiuchumi ya hadi shilingi bilino 62 kila mwaka,” alisema Kagwe.
Waziri Kagwe aliandamana na makatibu Dk. Kipronoh Rono wa kilimo, Jonathan Mweke wa ustawi wa mifugo na maafisa wa ngazi za juu katika wizara ya kilimo.