Kagwe asema utoaji chanjo utakuwa hiari, umma kuhamasishwa

Martin Mwanje
2 Min Read
Mutahi Kagwe - Waziri mteule wa Kilimo

Waziri mteule wa Kilimo Mutahi Kagwe amesema wakulima watakuwa huru kuamua ikiwa wanataka mifugo wao kuchanjwa au la punde mpango wa utoaji chanjo utakapong’oa nanga. 

Mpango huo ulikuwa umepangwa kuanza mwezi huu.

Akizungumza wakati akisailiwa na Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Taifa leo Jumanne, Kagwe hata hivyo ameelezea haja ya kuwahamasisha wakulima juu ya mpango huo kabla ya uzinduzi huo.

Alisema uhamasishaji huo unapaswa kuhusisha washikadau wote katika sekta ya kilimo ili kuelezea kwa mapana na marefu chanjo inayotumiwa na manufaa ya kuwachanja mifugo.

Kulingana na Kagwe, hatua hiyo itawawezesha wakulima kufanya uamuzi uliojikita kwa uelewa.

Serikali inakusudia kuwachanja ng’ombe milioni 22 na mbuzi na kondoo milioni 50.

Awali, Rais William Ruto alikuwa mstari wa mbele kupigia debe utoaji chanjo kwa mifugo.

“Ili kuhakikisha wakulima wanafaidika kikamilifu kutokana na fursa za kimataifa, tutatekeleza mpango mpana wa utoaji chanjo, kwa kutumia chanjo zilizozalishwa humu nchini, ili kupunguza kuenea kwa maradhi kwa mujibu wa viwango vya kimataifa,” alisema Rais Ruto wakati wa Tamasha la Kitamaduni la Baringo na Mnada wa Mbuzi wa Kimalel.

Kulingana naye, mpango wa utoaji chanjo kwa mifugo unalenga kukabiliana na maradhi kama vile ugonjwa wa miguu na midomo.

“Wale wanaopinga mpango huo hawana sababu na labda hawana ng’ombe. Wakati tunapokuwa na mazungumzo kuhusu ng’ombe, fyata tu ulimi ikiwa hauna ng’ombe,” alisema Rais Ruto.

Aliongeza kuwa chanjo itakayotumiwa ni ile inayozalishwa na Taasisi ya Uzalishaji wa Chanjo za Mifugo nchini Kenya (KEVEVAPI) na ambayo huzalisha chanjo za mifugo ambazo ni salama kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi nchini.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amekuwa mstari wa mbele kupinga mpango wa kuwachanja mifugo mwezi huu akitilia shaka usalama wa chanjo itakayotumika.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *