Wenyeji wenza wa fainali za Kombe la Dunia Mexico, walianza vyema safari yao ya fainali za 23, walipoikung’uta Afrika Kusini mabao 2-0 katika mchuano wa kundi A uliotitigwa mbele ya mashabiki wapatao 80,000 katika uwanja wa Mexico City.
Julian Quinones alipachika bao la kwanza katika Kombe la Dunia mwaka huu kunako dakika ya nane na kuwaweka wenyeji uongozini.
Javier Aquire aliongeza la pili lililowahakikishia El Tri, ushindi maridhawa.
Hata hivyo, wachezaji watatu walilishwa kadi nyekundu; Sphephelo Sithole na Themba Zwane wote wa Afrika Kusini na beki Ceasar Montes wa Mexico na kutimuliwa uwanjani kwa kucheza rafu.

Kabla ya kipenga cha kwanza kupulizwa, kulikuwa na sherehe za kufana za kufungua mashindano hayo zikiongozwa na wasanii mbalimbali wa nyumbani na wale wa kimataifa, wakiwemo Shakira na Burna Boy.
Ni mara ya tatu kwa Mexico kuandaa Kombe la Dunia baada ya mwaka 1976 na 1980.