KAA yaanzisha mpango wa kutuza watendakazi waadilifu

Marion Bosire
2 Min Read

Mamlaka inayosimamia viwanja vya ndege nchini, KAA imeanzisha mpango wa kutuza wafanyakazi wake waadilifu. 

Mpango huo utafanyika kila robo ya mwaka ili kutambua kujitolea kwao na ubora wa kazi zao.

Tuzo za kwanza kabisa chini ya mpango huo zimetolewa kwa wafanyakazi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Moi, MIA huko Mombasa na utakuwa ukitekelezwa pia katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Utambuzi huo wa wafanyakazi waadilifu ni sehemu ya mpango mkubwa wa tuzo za KAA za kuboresha huduma katika viwanja vya ndege unaolenga kuweka mazingira ya mashindano na kuhimiza uboreshaji endelevu wa huduma zinazotolewa katika viwanja vyote vinavyosimamiwa na KAA.

Katika utoaji wa tuzo hizo huko MIA, walinzi, wanaohudumia wateja na wahudumu katika idara mbalimbali waliangaziwa ambapo mlinzi Beatrice Weru alitambuliwa kama mshindi wa tuzo kuu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KAA Henry Ogoye alisema kwamba wamejitolea kutambua na kutuza wanaodhihirisha bidii kazini na wanaopenda kazi yao.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na maafisa wakuu wa KAA kama Meneja Mkuu wa Mipango na Usalama Harrison Machio, kaimu Meneja wa Mauzo na Maendeleo ya Biashara Angela Tilitei na Meneja wa Eneo la Pwani Abel Gogo.

Uwepo wao ni dhihirisho la kujitolea kwa KAA kutambua na kutuza mashujaa katika viwanja vya ndege nchini.

Share This Article