Justin Muturi ateuliwa kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma

Martin Mwanje
1 Min Read

Wizara ya Utumishi wa Umma hivi karibuni itaongozwa na Waziri mpya.

Hii ni baada ya Justin Muturi kupandishwa ngazi kwa kuteuliwa kuongoza wizara hiyo katika uteuzi wa hivi punde uliofanywa na Rais William Ruto.

Ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa na bunge, basi atachukua mahali pa Moses Kuria ambaye ameondolewa katika wizara hiyo.

Katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa, Muturi alihudumu kama Mwanasheria Mkuu.

Hata hivyo, alipotangaza orodha ya kwanza ya mawaziri wateule wiki jana, Rais Ruto alitangaza kumteua aliyekuwa Waziri wa Biashara Rebecca Miano kuwa Mwanasheria Mkuu.

Hiyo ilimaanisha kuwa Muturi aliondolewa kwenye wadhifa huo, na wengi walisubiri kuona hatima yake wakati orodha nyingine ya mawaziri ingetangazwa.

Hata hivyo, wadhifa wa Mwanasheria Mkuu ungali wazi baada ya uteuzi wa Miano kubatilishwa. Miano ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Utalii.

Inatazamiwa kuwa Rais Ruto atajaza wadhifa huo katika uteuzi wake ujao wakati akiendelea na mchakato wa kubuni serikali ya muungano itakayoakisi sura ya taifa.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *