Juliana Kanyomozi atoa pole kwa wazazi waliopoteza wanao Kampala

Watoto wanne waliuawa kwa kudungwa kisu shuleni Ggaba jijini Kampala nchini Uganda.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii wa muda mrefu wa muziki nchini Uganda Juliana Kanyomozi, ametoa pole zake kwa wazazi walioathiriwa na kisa kilichotokea kwenye shule moja jijini Kampala.

“Moja ya hofu kubwa kwa mzazi ni kupokea simu ya kutisha kutoka shuleni kwamba jambo fulani limempata mtoto wako!!” Aliandika Kanyomozi kwenye akaunti yake ya Instagram chini ya picha ya mshumaa.

Aliendelea kwa kuombea wazazi hao faraja akisema, “Ee Mungu mpendwa, tafadhali wafariji wazazi waliopoteza watoto wao katika janga la shule ya Ggaba. Roho zao ndogo zipumzike mbinguni”.

Yapata siku mbili zilizopita, polisi nchini Uganda walitangaza mauaji ya watoto wanne wa umri wa kati ya miaka miwili na mitatu kwa kudungwa kisu.

Watoto hao, wavulana watatu na msichana mmoja walifariki papo hapo huku mshukiwa jamaa wa umri wa miaka 39 akikamatwa na maafisa wa polisi.

Mshukiwa huyo aliokolewa na polisi walipomkamata kwani wazazi waliojawa na hasira walikuwa na mpango wa kumteketeza.

Jamaa huyo anaripotiwa kuzuru shule hiyo ya chekechea ya Ggaba ambapo alitafuta ushauri kuhusu kusajili mwanawe huko akaambiwa arejee Alhamisi.

Aliporejea siku hiyo, alikwenda afisini ambapo alilipa ada ya usajili na kuvamia watoto hao mara moja ambapo aliua wanne. Kilichomsukuma kutekeleza kitendo hicho cha unyama bado hakijajulikana.

Share This Article