Juhudi za kusitisha mgomo wa matabibu zagonga mwamba

Tom Mathinji
1 Min Read
Matabibu washiriki mgomo Jijini Nairobi.

Mashauriano yanayoendelea baina ya serikali ya kitaifa, baraza la magavana na matabibu yameshindwa kutatua mzozo kuhusiana na mgomo wa matabibu hao ulioingia katika siku yake ya 52 leo.

Maafisa wa chama cha KUCO waliotarajiwa kutia saini mpango wa kurejea kazini wameishumu serikali kwa ubaguzi kuhusiana na madai kwamba imekataa kutimiza shinikizo za wanachama.

Viongozi wa chama cha matabibu waliokutana na maafisa wa wizara ya afya na baraza la magavana walidai kwamba mgomo huo hautakomeshwa hivi karibuni huku matabibu hao wanaogoma wakiendelea kususia kazi.

Katibu mkuu wa KUCO George Gibore na mwenyekiti Peterson Wachira pia walilalamikia kile walichokitaja kuwa hali ya serikali, baraza la magavana na tume ya mishahara na marupurupu, SRC, kuwabagua wanachama wao na kupunguza marupurupu ya wanagenzi.

Miongoni mwa shinikizo za matabibu hao ni kwamba wahudumu wa afya waliofanya kazi chini ya mpango wa huduma za afya kwa wote waajiriwe kwa masharti ya kudumu na pia kuimarishwa kwa marupurupu ya hatari za kikazi kwa matabibu wote.

Share This Article